Na. James
Waibina
Inawezekana ukawa ni mke wa
mtu au una mpenzi wako ambaye mna matarajio ya kufunga ndoa na kuishi pamoja.
Kuna wakati unaweza kujaribiwa na kujikuta ukikabiliwa na hatari ya kumsaliti mwenzi
wako. Kujaribiwa huko kunaweza kukutokea katika mazingira mbalimbali kutegemea
na maeneo yako ya kazi au mahali unapofanyia shughuli zako za kila siku. Kwa
mfano inaweza ikatokea umefahamiana na mwanaume mahali pako pa kazi, anaweza
kuwa ni mteja au mfanyakazi mwenzio. Inatokea siku moja anakualika kwa ajili ya
chakula cha mchana, baada ya mtoko huo, unajisikia kutoka naye kwa mara
nyingine.
Kutoka
kwenu mara kwa mara kwenda kupata chakula cha mchana, unagundua kwamba huyu
bwana ni mtu mwenye kiwango cha juu ya usikivu, katika mazungumzo yenu
anaonekana sana kwamba ni mwelewa na mwenye subira. Hana papara katika
kuzungumza na mara nyingi huwa ni msikilizaji. Huyu unaweza kumwita rafiki
ingawa ni wa jinsia tofauti, si dhambi kuwa na rafiki wa jinsia tofauti
bali urafiki huo unapaswa kuwa na mipaka.
Kuna kitu wenzetu wazungu
wanakiita Emotional infidelity, kwa tafsiri yangu naweza kusema ni hisia za
usaliti katika mapenzi. Maana yake ni kwamba unaruhusu mtu mwingine wa jinsi
tofauti azibe pengo la hisia ambalo lingetakiwa lizibwe na mpenzi wako au mume
wako.
Wanawake ni viumbe wa
hisia, wanapenda sana kusikilizwa, na wanapenda kuona wapenzi wao au waume wao
wanawasikiliza. Inapotokea hitaji hilo halitekelezwi na mpenzi au mume wake,
basi ni rahisi sana atakapotokea mtu mwingine ambaye bila kujua akamudu kuziba
pengo hilo kuvutiwa naye na kuhitaji kuwa naye karibu mara kwa mara.
Zifuatazo ni dalili ambazo zitakuonyesha kwamba ukaribu wako na rafiki uliyenaaye (jinsia tofauti) utakupelekea
kuisaliti ndoa yako:-
1. Unatamani sana kumuona
ukiwa na shauku kubwa ya kuwa naye karibu na kutumia muda mwingi kuwa
naye.
2. Unajikuta ukichagua
mavazi na kujikagua sana ukijiuliza jinsi atakavyo vutiwa na mavazi yako pale
atakapokuona.
3. Unapokuwa naye unajikuta
ukimweleza matatizo ya mahusiano yako na mpenzi wako au mumeo.
4. Unajikuta ukimgusa gusa
wakati mkiongea au kufanya naye utani unaoweza kupeleka ujumbe tofauti kwake
kwamba labda umevutiwa naye kimapenzi.
5. Unawasiliana naye kwanza
kabla ya kuwasiliana na mpenzi wako au mumeo pale unapokabiliwa na jambo lolote
lenye kutatiza na linalohitaji msaada wa haraka au ushauri.
6. Unajikuta ukiwaza jinsi
gani ungekuwa na amani iwapo ungekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi au ndoa.
7. Inawezekana ukawa
unamzuingumzia sana kwa mwenzi wako au kwa marafiki zako, au inawezekana ukawa
humzungumzii kabisaaa na kuficha urafiki wenu.
8. Unajitahidi sana kuficha
urafiki wenu na kutomzunguimzia rafiki huyo kwa mwenzi wako kwa sababu unajua
kwamba jambo hilo linaweza kukuletea balaa.
Kwa ujumla unapojikuta
umempata rafiki wa jinsia tofauti na yako halafu ukahisi kulipukwa na moyo juu
yake zikiwemo dalili nilizozitaja hapo juu, basi ujue uhusiano wako na mume au
mpenzi wako uko mashakani. Usipokuwa makini utamsaliti.
Kwa Ushauri au Maoni
yoyote, tuwasiliane kupitia +255 713 515 059 /+255 767 515 059 au barua pepe jameswaibina@fumbuka.co.tz
0 blogger-facebook:
Post a Comment